EAC YATAHADHARISHA KUHUSU EBOLA

Nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimehimizwa kuchukua tahadhari na
kuimarisha uratibu wa Mipaka kufuatia kuthibitishwa mlipuko mpya wa Virusi vya ugonjwa wa
Ebola (Ebola Bundibugyo EVD) katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mlipuko huo ulithibitishwa Mei 15, 2026 na Waziri wa masuala ya Afya wa nchi hiyo na kwamba
umejikita katika mkoa wa Ituri, mashariki wa DRC unaopakana na Uganda na Sudan Kusini.
Taarifa iliyotolewa Mei 18, 2026 na Sekretarieti ya EAC imeeleza kuwa ripoti zilizopo zinaonesha
kuwa hadi kufikia Mei 15, 2026 takribani visa 246 na vifo 65 vilikuwa vimeripotiwa, huku visa
viwili vya Ebola Bundibugyo vinavyohusishwa na wasafiri kutoka DRC, vikithibitishwa nchini
Uganda na kuripotiwa kwa kifo kimoja katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala.
Taarifa hiyo imemnukuu Naibu Katibu Mkuu wa EAC anayesimamia Miundombinu, Uzalishaji,
Jamii na Sekta za Kisiasa, Andrea Aguer Ariik Malueth akisema kuwa EAC itaendelea kuwa
macho na kujitolea kikamilifu kusauidia nchi wanachama katika kuimarisha uangalizi, uchunguzi
wa maabara, kinga na udhibiti wa maambukizi, mawasiliano ya hatari na ushirikishwaji wa jamii
hasa katika maeneo ya mipakani.
“Kutokana na harakati za kiwango cha juu cha watu na bidhaa katika eneo letu, maandalizi
yaliyoratibiwa na kubadilishana habari haraka ni muhimu kuzuia maambukizi ya mpakani na
kulinda afya na maisha ya wana Afrika Mashariki.” amesema Ariik.
Amezihimiza nchi wanachama wa jumuiya hiyo kuwezesha mipango na maandalizi ya kitaifa
hususani kuratibu uvukaji wa mipaka, kuimarisha uchunguzi na ufuatiliaji katika sehemu za
kuingilia na kuhakikisha wafanyakazi wa sekta ya afya na timu saidizi zinakuwa na vifaa na
weledi wa kugundua na kukabiliana na kesi zote zinazoshukiwa.
Virusi vya Ebola ni ugonjwa hatari na mara nyingi husababisha kifo. Huambukiza kwa kugusana
moja kwa moja na damu au maji maji kutoka mwili wa mtu aliyeambukizwa
Wanyama aina ya Nyani wanahusishwa moja kwa moja katika maambukizi ya Ebola.
Dalili za mapema za maambukizi ni pamoja na homa ya ghafla, udhaifu wa mwili, maumivu ya
kichwa, maumivu ya misuli na koo, ambayo hufuatiwa na kutapika, kuhara, maumivu ya tumbo
na katika baadhi ya matukio kutokwa na damu katika sehemu mbalimbali za mwili kulingana na
aina ya Virusi.
Mlipuko wa sasa ni wa 17 wa Ebola uliorekodiwa nchini DRC tangu ugonjwa huo
ulipotambuliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976 karibu na Mto Ebola.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *