NCHIMBI AIWAKILISHA TANZANIA MKUTANO WA OACPS

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Dkt. Emmanuel
Nchimbi, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia
Suluhu Hassan katika Mkutano wa 11 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Jumuiya
ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS), uliofanyika nchini Guinea ya
Ikweta.
 
Katika ufunguzi wa Mkutano huo uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha
Kimataifa cha Sipopo kilichopo jiji la Malabo nchini Guinea ya Ikweta, Viongozi
kutoka nchi mbalimbali wamehimiza umuhimu wa hitaji la kufanya mageuzi ya
Kitaasisi na kimfumo, kuwezesha Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki
(OACPS), kukabiliana na changamoto zinazoikabili Dunia kwa sasa ikiwemo,
migogoro ya kisiasa, vita pamoja na mabadiliko ya tabianchi.
 
Aidha, mkutano huo umesisitiza umuhimu wa kukuza biashara baina ya nchi
wanachama pamoja na jumuiya nyingine za kikanda, na kuwajengea uwezo vijana
na wanawake ili waweze kushiriki vema katika shughuli za maendeleo.
Pia umetolewa wito na mkazo kwa nchi wanachama kutoa michango kwa wakati,
ili kuifanya Taasisi ya hiyo kujitegemea kifedha na kuwa sauti huru kwenye
jumuiya ya kimataifa. 
Ushiriki wa Tanzania katika Mkutano huo ni mwendelezo wa jitihada za kuendelea
kushiriki kikamilifu katika majukwaa ya kikanda na kimataifa, na kudhihirisha
mchango wa nchi katika mijadala ya maendeleo na ushirikiano wa kimataifa.
 
Katika Mkutano huo, Rais wa Angola, Joao Manuel Lourenzo, amekabidhi
Uenyekiti wa Jumuiya hiyo kwa Rais wa Guinea ya Ikweta,Teodoro Obiang
Nguema Mbasogo.
 
Jumuiya ya Nchi za Afrika, Karibiani na Pasifiki (OACPS) yenye jumla ya nchi
wanachama 79 na rasilimali watu bilioni 1.5, ilianzishwa miaka ya 1970 kwa lengo
la kuzisaidia kiuchumi na kisiasa nchi zilizopo Afrika, Karibiani na Pasifiki
zilizotawaliwa na nchi za Bara la Ulaya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *