KWAHERI MZEE EDWIN MTEI

Na Angelo Mwoleka,

Kati ya mwaka 2007 hadi 2011 nilikuwa mtayarishaji na muendeshaji wa kipindi cha MEDANI ZA SIASA NA UCHUMI cha Star Tv, na miongoni mwa watu niliofanya nao vipindi mara nyingi ni Mzee Edwin Mtei.

Hakuwahi hata siku moja kunikatalia kushiriki kipindi kila nilipomhitaji, na wakati wote tulilazimika (mimi na mpiga picha wangu Ramadhan Mvungi) kwenda kurekodi kipindi nyumbani kwake Ogaden Estate, karibu na Tengeru umbali wa kilometa 13 kutoka jijini
Arusha.

Mzee Mtei hakuwa mshiriki tu wa kipindi, bali alikuwa mwalimu wa historia na siasa za Tanzania, kwani kila aliposhiriki alitoa darasa la kutosha kuhusu Mipango na Uchumi na kuipa siasa nafasi ndogo. Ni kwa sababu hiyo nilimuomba msimamizi wa Uzalishaji Maudhui wa vipindi Star Tv (Paul Mabuga) kubadilisha jina la kipindi kutoka MEDANI ZA SIASA na kukiita MEDADI ZA SIASA NA UCHUMI (ingawa sasa kimerudishwa jina la zamani la Medani za Siasa).

Kupitia uzoefu wake wa utumishi na nyadhifa mbalimbali alizoshika serikalini na nje ya serikali ikiwemo Gavana wa kwanza wa Benki Kuu ya Tanzania, Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alitumia kipindi cha Medani za Siasa na Uchumi kuelimisha jamii kuhusu misingi na fursa za maendeleo kulingana na nyakati.

Kwa upande wa Siasa, Mzee Mtei pamoja na kuwa miongoni mwa waasisi wa mageuzi nchini na mwasisi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alisisitiza umuhimu wa kuzingatia malengo ya uanzishwaji wa vyama vingi vya siasa, na kusisitiza serikali na chama tawala kupokea maoni na ushauri wa vyama vya upinzani na kuyafanyia kazi kwa manufaa ya taifa badala ya kuwachukulia kama maadui.

Hayati Edwin Mtei (kulia) enzi ya uhai wake akiwa na Mwandishi wa Habari, Angelo Mwoleka

Nakumbuka mwaka 2011 nilimuomba Mzee Mtei kushiriki kipindi pamoja na kijana kutoka Chama cha Mapinduzi-CCM ili kuunganisha mawazo na mitazamo, alinikubalia. Niliwaweka meza moja na hayati Alphonce Mawazo, ambaye wakati huo alikuwa Diwani wa Kata ya Sombetini jijini Arusha. Baada ya kumaliza kipindi alimwambia Mawazo maneno ambayo nayakumbuka vizuri:

“Wewe kijana una akili nzuri sana na pia una mawazo mazuri kama jina lako. Natamani nchi hii tungekuwa na vijana wengi kama wewe wenye mitazamo ya kimaendeleo na demokrasia, lakini bahati mbaya upo CCM, nawajua vizuri hayo uliyoyasema hapa huwezi kwenda kuyasema au kushauri huko, watakushughulikia, nakushauri njoo Chadema.”

Na kweli siku chache baadae Mawazo alihamia Chadema kabla ya kuuawa huko mkoani Geita katika mazingira ya kutatanisha.

Kwaheri mzee Edwin Mtei, taarifa ya kifo chako iliyotolewa jumanne Januari 20, 2026 imenikumbusha mengi, siyo tu ushiriki wa kipindi cha Medani za Siasa na Uchumi bali pia ukarimu wako na mke wako kila tulipofika nyumbani kwako Ogaden Estate.

Sitasahau ulivyokuwa ukinitembeza kwenye mabanda ya Nguruwe na Ngombe huku ukinishawishi kufanya biashara ya ufugaji wa Nguruwe, ukiahidi kunipa watoto watatu (Piglets) kama kianzio lakini bahati mbaya sikuwa na utayari.

Wakazi wa Arusha hususani watumiaji wa usafiri wa umma, maarufu kama Daladala watakukumbuka kila jina lako litakapotajwa wakati wa kushusha au kupakia abiria mbele ya lango la kuingia shambani kwako, ambapo kuna kituo maarufu cha daladala kiitwacho KWA MTEI.

Kwaheri mzee wetu Edwin Mtei, pumzika kwa amani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *